Wednesday, May 16, 2012

MICHANGO YA SHULE YAMKWAMISHA KUJIUNGA NA SECONDARY HANDENI



Mwanafunzi Mwenjuma M. Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Komnyanganyo wilayani Handeni akimuonesha mwandishi fomu ya kuitwa shuleni.
Mwenjuma M. Magalu (kulia) akiwa na Bibi yake nyumbani kwao Kijiji cha Msasa, wilayani Handeni.
Mama wa mtoto huyo Bi. Hadija Magalu.


Licha ya Serikali kuliarifu Bunge la Tanzania kuwa wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba mwaka 2011 kutoka mikoa 12 tayari wamejiunga na kidato cha kwanza, imebainika bado kuna wanafunzi wameshindwa kujiunga na shule kutokana na kipato duni cha familia zao.

Mmoja wa wanafunzi hao Mwenjuma Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Komnyang’anyo wilayani Handeni ni miongoni mwa wanafunzi walioshindwa kujiunga na sekondari kutokana na mama yake kushindwa kumgharamia mahitaji ya shule.

Akizungumza hivi karibuni kijijini Msasa, wilayani Handeni katika utafiti uliofanyika kwa ushirikiano na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), mama wa mtoto huyo Hadija Magalu aliyetelekezwa na mumewe kwa muda mrefu amesema ameshindwa kumsomesha mwanaye kutokana na kipato duni alichonacho.

Magalu amesema alipata taarifa za kufaulu kwa mwanae tangu Desemba 12, 2011 na kuanza kujikusanya taratibu lakini hadi muda wa kwenda shule ulipofika (Januari 9, 2012) alikuwa hajakamilisha baadhi ya vifaa vinavyohitajika shuleni vikiwemo fedha ya ada na michango mingine.

Michango iliyomkwamisha mwanafunzi Mwenjuma Magalu kujiunga na kidato cha kwanza ni ada ya sh. 20,000, fedha ya taaluma sh. 10,000, fedha ya madawati 15,000, fedha ya sweta sh.10,000, kitambulisho sh. 5,000, ulinzi sh. 5,000, tahadhari 5,000 pamoja na fedha kwa ajili ya nembo ya shule sh. 2,000.

Akihutubia Mkutano wa Saba wa Bunge la Tanzania lililomalizika hivi karibuni, Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kutoka mikoa 12 ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mara, Morogoro, Mwanza, Lindi, Kilimanjaro, Pwani, Ruvuma  na  Tanga, wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba wamefanikiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Hata hivyo mwanafunzi Magalu kwa sasa anafanya vibarua kwa moja ya kampuni za Kichina zinazofanya ujenzi wa barabara inayopita Kijiji cha Msasa, kwa madai anatafuta fedha za ada na endapo akikamilisha atahakikisha anaendelea na elimu ya sekondari hapo baadae.

Mwandishi wa habari hizi alipojaribu kuzungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni Hassan Mwachibuzi alisema ofisi yake haina taarifa za mtoto huyo kushindwa kujiunga na shule, hivyo kumshauri mwandishi amueleze mtoto huyo kufika ofisi za halmashauri ili aweze kujieleza na ikiwezekana kusaidiwa.

Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA).


No comments:

Post a Comment