Tuesday, May 22, 2012

Sera Zinatubana Kusomesha Wanafunzi Waliozaa Handeni


 Mratibu wa Elimu Kata ya Chanika, Ramadhan Majogo.
    Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Handeni na Ofisa Elimu Sayansi Kimu Handeni, Ester Ngao.
----

 Na Joachim Mushi

HALMASHAURI ya Wilaya ya handeni imesema ipo tayari kuanza kuwasaidia kielimu wanafunzi waliopata mimba na kukatisha masomo, endapo Serikali itapitisha rasmi sera ya kuridhia kundi hilo la wanafunzi kuendelea na masomo katika mfumo wa elimu ya kawaida.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Ramadhan Diliwa alipokuwa akizungumza na Thehabari.com kwa simu kufafanua mfuko wa elimu wilaya hiyo unavyotumiwa kuzisaidia familia zinazoshindwa kulipia gharama za elimu.

Mwenyekiti Diliwa alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuelezwa kuwa wapo baadhi ya wasichana ambao walirubuniwa wakiwa shuleni na kutiwa mimba kabla ya kukatishwa masomo, na sasa baadhi wapo tayari kurejea shuleni.

Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na mwandishi wa habari hizi kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), umebaini uwepo wa idadi kubwa ya wasichana wanaokatishwa masomo kwa mimba jambo ambalo linaharibu maendeleo ya elimu eneo hilo.

Akifafanua zaidi Diliwa alisema halmashauri hiyo ipo tayari kuwasaidia wanafunzi hayo kupitia mfuko wa elimu wa wilaya hiyo, lakini kikwazo ni sera za Serikali bado hazijaridhia kitu kama hicho.

"Tunaweza kuwasaidia kundi hilo (wanafunzi waliopata mimba), lakini yapo masuala mengi ya kuangalia, je itawezekana kwa utaratibu gani na sera zinaruhusu kufanya hivyo...maana nilikuwa nasikia watu wakiizungumzia kuwa kundi hilo liendelee na masomo baadaye lakini sera bado hazijaridhia," alisema Diliwa.

Aidha aliongeza kuwa kwa sasa mfumo huo umewalipia gharama za masomo wanafunzi takribani 240 katika hatua balimbali za masomo, hivyo kuwahimiza familia ambazo zinakwama kabisa kuwalipia watoto wao ada wasiogope kuja ofisini ili watambuliwe kabla ya kuanza kusaidiwa.

Pamoja na halo ameitaka jamii kuacha kutoa visingizio vya wanafunzi kutiwa mimba kwa kile kutokuwepo kwa mabweni katika shule nyingi za kata, kwani hata zamani kulikuwa na shule za bweni lakini wapo baadhi ya wanafunzi walitiwa mimba.

*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa  www.thehabari.com kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA).

No comments:

Post a Comment