Friday, May 25, 2012

MZUMBE YAINGIA UBIA NA VYUO VIKUU VYA NJE


CHUO Kikuu cha Mzumbe cha mkoani hapa kimesaini makubaliano pamoja na vyuo vingine vitatu vya nje ya nchi wa kuendesha kozi ya Shahada ya Pili ya Utawala na Menejimenti kwa watumishi wa sekta ya afya wakiwa kazini. 
Watumishi wa Sekta ya Afya wa hapa nchini pamoja na Kenya, Rwanda, Malawi na Cameroon watanufaika na kozi hizo. 
Licha ya Mzumbe, vyuo vingine vilivyoingia makubaliano hayo ni Chuo Kikuu cha Hochuschule Neu –Ulim (HNU) cha Ujerumani, Chuo Kikuu cha Chepkoiel kutoka Kenya. 
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano ya uendeshaji wa kozi alisema watakaohusika ni wafanyakazi waliopo kazini wenye sifa watakaosoma MBA kwa kipindi cha miaka mitatu. 
Alisema idadi ya watumishi wa sekta ya afya wenye sifa watakaokuwa wakinufaika na mpango huo ni kuanzia 20 hadi 30 na masomo hayo yanatarajia kuanza rasmi mwakani. 
Alisema, awali Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo cha HNU walitiliana mkataba miaka miwili iliyopita kuendesha programu hiyo ambapo wanafunzi walikuwa wakienda kusoma Ujerumani na wahitimu wa kwanza ilikuwa Juni mwaka jana na kundi la pili linatarajiwa kuhitimu mwezi ujao. 
Chuo Kikuu Mzumbe na HNU kutokana na kuona gharama ni kubwa za uendeshaji viliamua kutafuta mbia ambapo Chuo Kikuu cha Chepkoilel cha Nairobi kilikubali kuwa mshiriki na hivyo kusainiwa mkataba wa kuendeshwa kozi hiyo kwa ubia wa vyuo vitatu vitakavyotoa wataalamu wa kufundisha. 
Rais wa Chuo Kikuu cha HNU cha Ujerumani, Profesa Uta Feser alisema kuanzishwa kwa programu hiyo katika Afrika kutazisaidia nchi mbalimbali kunufaika kwa kuwasomesha wataalamu wao.

No comments:

Post a Comment