Saturday, May 26, 2012

TAIFA STARS KUPAMBANA NA MALAWI DAR LEO.


Timu ya taifa ya Tanzania (taifa stars)
 Timu ya taifa ya Malawi (The Flame)
Timu za Taifa za Tanzania (Taifa Stars) na Malawi (The Flames) zinapambana leo (Mei 26 mwaka huu) katika mechi ya kirafiki itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Makocha wa timu zote mbili, Kim Poulsen wa Taifa Stars na Kinnah Phiri wa The Flames wamezungumzia umuhimu wa mechi hiyo katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Jana (Mei 25 mwaka huu) ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kim ambaye hiyo itakuwa mechi yake ya kwanza tangu asaini mkataba wa kuinoa Stars, amesema baada ya mazoezi ya siku kumi hicho ndicho kipimo chake cha kwanza na cha mwisho kabla ya kucheza na Ivory Coast kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayofanyika ugenini Juni 2 mwaka huu.
“Wachezaji wangu wamekuwa wakipokea mafunzo vizuri ingawa Nurdin Bakari na Thomas Ulimwengu hatakuwepo kwa vile ni majeruhi. Bila shaka baada ya mazoezi ni lazima ujipime, hivyo mechi hii ni muhimu kwangu ukizingatia kuwa kwenye ubora wa viwango vya FIFA, Malawi wako juu yetu,” amesema Kim 
Naye Phiri ambaye ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Malawi amesema awali aliombwa mechi na Misri, lakini akaamua kucheza na Taifa Stars kwa vile anaamini kitakuwa kipimo kizuri kwake kabla ya kucheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Kenya itakayofanyika Juni 2 mwaka huu jijini Nairobi.
“Nimekuja na wachezaji 20 ambapo nusu yao wanacheza mpira wa kulipwa nje ya Malawi, wengi wakiwa Afrika Kusini lakini wapo pia kutoka Msumbiji na mmoja anacheza Hispania katika timu ya vijana ya Atletico Madrid. Tumejianda si kwa mechi hii tu, bali pia dhidi ya Kenya na baadaye Nigeria ambao tutacheza nao numbani Juni 9 mwaka huu,” amesema Phiri ambaye kwenye benchi lake la ufundi anasaidiwa na Young Chimodzi.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 3,000 kwa viti vya kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A inayochukua watazamaji 748 tu itakuwa sh. 20,000.

No comments:

Post a Comment