Baada
ya kuwapo kwa amani kwa takribani mwaka mmoja tangu kuundwa kwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, vurugu na hali ya wasiwasi
zimeibuka tena baada ya wanaharakati wa Kiislam kufanya maandamano
kutaka uhuru wa visiwa hivyo.
Zanzibar
ilijikuta katika hali tete kiusalama tangu mwaka 1995 baadaya
kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais, ambayo Chama cha Mapinduzi
(CCM) kiilibuka kidedea na Chama cha Wananchi (CUF) kupinga, lakini
uhasama huo ulizikwa Julai 31 mwaka 2010, baada ya kura ya maoni ya
kuunda Serikali hiyo ya umoja wa kitaifa.
Lakini
kuanzia juzi usiku hadi jana jioni mji wa Unguja na viunga vyake
ulitikiswa na mabomu ya kutoa machozi ambayo polisi waliyatumia
kutawanya mamia ya wanaharakati hao wa Kiislam wakiongozwa na Jumuiya ya
Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI).
Mabomu
ya machozi yalipigwa mfululizo juzi usiku na kuendelea kutwa nzima
jana, hivyo kuathiri shughuli za biashara, ibada katika makanisa
mbalimbali na kusababisha hofu kwa wananchi.
Kwa
muda wa saa takriban mbili hivi kati ya saa 3:00 na saa 5:00 asubuhi,
helkopta ya polisi ilikuwa ikipasua anga la Zanzibar ambalo lilikuwa
limetandwa na moshi uliotokana na mabomu ya machozi pia uchomaji wa
matairi ya magari.
Kamishna
wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa aliwaambia waandishi wa
habari kuwa wafuasi hao wamefanya uharibifu mkubwa ikiwa pamoja na
kuchoma moto makanisa mawili na kwamba, watu saba akiwamo Imamu wa
Msikiti wa Bizeredi, Maalim Mussa Juma wanaotuhumiwa na matukio hayo
wamekamatwa na jeshi hilo.
Akizungumza
na Mwandishi wa habari hizi Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies
of God (TAG), Askofu Dickoson Maganga alisema watu wasiojulikana
walivamia kanisa lao eneo la Kariakoo Mjini Zanzibar mnamo saa 4.30
usiku na kuvunja ukuta, kuchoma viti vya plasitiki pamoja na gari yake.
Chanzo
cha vurugu hizo kinatajwa kuwa ni wanaharakati hao juzi kufanya
mkusanyiko na maandamano makubwa ya kushtukiza ambayo yalizistua mamlaka
za usalama visiwani humo, lakini baada ya kutawanyika jioni baadhi ya
viongozi wa maandamano hayo walitiwa mbaroni.
Baada
ya kukamatwa kwao, wafuasi wao walikusanyika makao makuu ya polisi Mkoa
wa Mjini Mharibi, Madema, kushinikiza kutolewa kwa viongozi hao
wanaoshikiliwa kituoni hapo.
Habari
zaidi zinasema kutokana na hali ilivyo, askari polisi walitarajiwa
kuongezwa visiwani humo, ili kusaidia kuimarisha hali ya usalama pia
kuwadhibiti wahalifu ambao walikuwa wameanza kuelekea nje ya maeneo ya
mji.
Tayari
kuna taarifa kuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) kutoka Tanzania bara jana mchana walingia Zanzibar kwa ajili ya
kuongeza ulizi katika mji wa Unguja.
Hata
hivyo, katika hali ya kushangaza hakuna kiongozi yoyote wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) aliyetoa kauli kuhusu hali hiyo.
Kamishna
Mussa alisema jeshi lake litaendelea kuwasaka na kuwatia mikononi wote
waliopanga fujo hizo pamoja na viongozi wote wa JUMIKI.
“Jumuiya
ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar ndio iliyohusika na
kuwachochea vijana kukusanyika na kufanya uharibifu ikiwemo kuchoma moto
gari, kupanga mawe barabarani na kufanya hujuma mbalimbali kinyume cha
sheria. Tutaendelea kuwasaka kwa gharama zote,” aliapa Kamishna Mussa.
Alifafanua
kwamba kwa sasa mikusanyiko yote ya mihadhara ya kidini na vyama vya
siasa, lazima ipate kibali cha polisi vyinginevyo jeshi lake litatumia
nguvu za ziada kutawanya mikusanyiko hiyo ili kulinda sheria za nchi,
amani na utulivu.
Hata
hivyo, kamishna huyo wa polisi alijizuia kuhusisha harakati za Uamsho
na chama cha siasa wala kutaja majina ya viongozi ambao tayari
wanashikiliwa na jeshi lake.
“Mpaka
sasa hivi sina majina yao kwa jumla, lakini tumewakamata viongozi wa
Uamsho na tunatendelea kuwasaka lakini jina moja tu ndio ninalo ambalo
ni Mussa Abdallah Juma,” alisema Kamishna huyo.
No comments:
Post a Comment