Sunday, May 20, 2012

RUSHWA YA NGONO IMEKITHIRI VYUO VIKUU

Fatma at Dar es salaam
LEO wazalendo wenzangu nina mada ambayo imejificha kidogo, ambayo imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya taifa kwa namna moja.

Kama macho yako yatakuwa yametazama kichwa cha habari hapo juu, utakuwa pamoja nami na kufahamu nini nataka kuzungumzia.

Jana katika harakati za shughuli zangu za kila siku niliweza kutembelea moja ya chuo cha elimu ya juu hapa nchini. Mandhari ya chuo hicho ni mazuri yanayovutia sana, binafsi nimevutiwa na hali ya usafi wa mazingira ya chuo hicho. Nilikuta wanafunzi wakijisomea makundi kwa makundi, wanawake na wanaume.

Kuna malalamiko kuwa eti baadhi ya wahadhiri wa vyuo vikuu huwa wanataka wapewe rushwa ya ngono ili watoe majibu ya mitihani kwa wanafunzi wanawake!

Hili ndilo lililopelekea mimi kufanya uchunguzi ili niweze kugundua ukweli wa mambo. Najua yawezekana kama wewe ni mwanafunzi mwanamke umewahi kukutana na tatizo hili!
Naamini kabisa wapo baadhi ya wanafunzi wanaokubali kutoa rushwa ya ngono ili waweze kufaulu lakini wengi wao hawapendi kitendo hicho cha udhalilishaji.

Nikafika chini ya mti mmoja ambao walikuwa wameketi wanafunzi wanawake na kuwasabahi kabla ya kuanza uchunguzi wangu juu ya jambo hilo.

Wakanieleza kuwa tatizo la rushwa ya ngono lipo na wahadhiri wanalitumia kama silaha pekee kufanikisha jambo hilo.

Mmoja wa wale wanafunzi alisema, “yaani hata ukiwa na rafiki yako wa kiume ni tatizo, mnaweza kufelishwa mitihani yenu kwa sababu eti umekataa kutembea na mhadhiri!”
Tatizo la rushwa ya ngono lipo karibu vyuo vingi vya elimu ya juu hapo nchini, lakini hebu tujiulize ni hatua gani zimechukuliwa mpaka sasa!

Kuna malalamiko mengi katika vyuo kuwa baadhi ya wahadhiri wana tabia ya kuwataka kimapenzi wanafunzi wa kike ili waweze kuwapa majibu ya mtihani.

Malalamiko ya wanachuo ambao wanatakiwa kutoa rushwa ya ngono yanapopelekwa hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya hao, hilo ni tatizo ambalo linapaswa kutafutiwa dawa.

Labda tujiulize wanavyuo ambao wanahitimu na kuvishwa joho kubwa huku wazazi wao wakiwavisha mashada ya maua wakati wanatambua kuwa wapo waliofaulu kwa kutoa miili yao wanajisikiaje?

Wahadhiri ambao wanafanya vitendo hivyo nao wanajisikiaje? Ni wazi kila mmoja atakuwa na haya katika moyo wako hata kama akijitahidi kuificha aibu katika macho yake.
Kwa kitendo hicho kinachofanywa na baadhi ya wahadhiri wachache ambao wanakiuka maadili ya kazi yao ni kukosa uzalendo.

Inawezekana kabisa hao waliotoa rushwa ya ngono na kufaulu kwa kiwango cha juu hawawezi kumudu vyema taaluma waliyoisomea, matokeo yake tunakuwa na wataalamu wababaishaji.

Wale ambao walipinga rushwa ya ngono kwa nguvu zao zote na wakaamua kujituma watafaulu, tena yawezekana kwa alama za juu kuliko hao waliotoa rushwa ya ngono.
Naamini kila mmoja anatambua kuwa Rais wetu wa kwanza Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kuwa rushwa ni adui wa haki.

Ni jambo la aibu kwa mhadhiri aliyesomeshwa kwa fedha nyingi za walipa kodi wa nchi yetu kufanya kitendo cha namna hii.

Kwani atasababisha tuwe na wataalamu ambao hawana viwango vizuri na kupelekea afanye kazi chini ya kiwango.

Na wewe mhitimu ambaye umemaliza chuo kikuu na kufaulu kwa kutoa mwili wako, unapaswa kutambua kuwa hujaitendea haki nchi yako pamoja na wazazi wako.
Kwa sababu hutokuwa na uwezo mkubwa katika fani uliyoisomea matokeo yake utafanya kazi kwa ubabaishaji.

Hatimaye utalitia hasara Taifa kwa namna moja, mfano ukiwa mwalimu utafundisha chini ya kiwango na kusababisha wanafunzi wengi wafeli.

Yawezekana ukawa daktari ukasababisha kutoa matibabu chini ya kiwango na kusababisha kifo kwa mgonjwa.

Pengine ukawa mhasibu ukapelekea hasara katika idara fulani ya serikali kwa kuwa huna utaalamu wa kutosha bali ulifaulu kwa kupewa mitihani baada ya kutoa rushwa ya ngono.
Katika tatizo hili la kutoa rushwa ya ngono katika vyuo vyetu vikuu serikali inapaswa kulitazama hili kwa makini.

Kuna hasara nyingi zinazotokea hapo baadae ukiangalia kwa kina jambo hili. Ni vema hatua kali zichukuliwe kwa baadhi ya wahadhiri wanaotaka kuhongwa ngono na wanavyuo wanaokubali kutoa rushwa ya ngono.

Kuweni wazalendo, tambueni mnachokifanya ni kinyume na maadili ya taaluma yenu, ni aibu kwa hayo mnayofanya mbele ya jamii.

Wanavyuo mnaoshiriki kutoa rushwa ya ngono pia mnajidhalilisha na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa. Hata kama ikiwekwa sheria kali ya vitendo hivi bila ya wahusika kubadilika itakuwa ni kama kutwanga maji kwenye kinu.
Sereva20002@yahoo.co.uk


1 comment:

  1. well said girl:)the problem is that we are passing exams bt we are not educated.
    we are going to school but school does nt humanize us contrary it dehumanize us.
    #tafakari.

    ReplyDelete