Tuesday, June 12, 2012

TAMKO LA SERIKALI DHIDI YA MALALAMIKO YA MATOKEO KIDATO CHA SITA 2012

NECTA'S LOGO
TAMKO LA SERIKALI KUHUSU MALALAMIKO DHIDI YA MATOKEO YA SOMO LA ISLAMIC KNOWLEDGE KATIKA MTIHANI WA
KIDATO CHA SITA 2012


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

1.0 UTANGULIZI
Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha sita 2012 yaliyotangazwa rasmi tarehe 01/05/2012. Tarehe 28/5/2012 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilipokea barua kutoka Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu yenye Kumb. Na. BSK/W/012/01 ya tarehe 22/5/2012 iliyoeleza kutoridhika na ufaulu wa watahiniwa waliofanya somo la Islamic Knowledge kwa kuwa waliona matokeo yaliyotangazwa hayakuwa na uhalisia wa uwezo wa wanafunzi. Kutokana na barua hiyo, Serikali ilifanya uchunguzi kwa kuangalia mambo yafuatayo:
 Kulinganisha alama za watahiniwa zilizojazwa katika vituo vya usahihishaji mitihani na zile zilizohifadhiwa katika Kompyuta, yaani database ya Baraza la Mitihani ili kubaini kama kuna tofauti yoyote; na
 Kulinganisha alama za somo la Islamic Knowledge zilizochakatwa na Mfumo wa Kompyuta na sampuli ya alama zilizokokotolewa kwa kutumia kikokotozi (calculator).

2.0 MATOKEO YA UCHUNGUZI
 Baada ya kupitia hatua za uhakiki kuhusu usahihishaji na utoaji wa matokeo, ilibainika kuwa alama za mwisho katika somo la Islamic Knowledge zilizokokotolewa na Mfumo wa Kompyuta ZILITOFAUTIANA na alama zilizopatikana kwa kutumia kikokotozi. Uchunguzi zaidi uliofanyika kwa lengo la kubaini chanzo cha tatizo katika uchakataji wa matokeo hayo
kwenye Mfumo wa Kompyuta ulionesha kuwa uchakataji uliotumika awali kutoa matokeo ya mwaka 2012 ulitumia jumla ya “Paper” tatu kama ilivyokuwa mwaka 2011.

 Kutokana na mabadiliko ya Fomati ya Mtihani wa somo la Islamic Knowledge yaliyoanza kutumika rasmi katika Mtihani wa Kidato cha Sita 2012, mtihani huo kwa sasa una “paper” mbili na siyo “paper” tatu. Hivyo, tofauti ya alama iliyobainika imetokana na Mfumo wa Kompyuta kuendelea kutumia “paper” tatu katika kupata wastani wa alama za mwisho badala ya kutumia “paper” mbili.

3.0 HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI
 Baada ya kugundua dosari hiyo kwa somo la Islamic Knowledge, uhakiki ulifanyika kwa masomo yao yote ya Mtihani wa Kidato cha Sita 2012 yaliyokuwa na “paper” zaidi ya moja ili kujiridhisha endapo uzito sahihi ulitumika katika kupata wastani wa alama za watahiniwa. Matokeo ya uhakiki huo yalionesha kuwa alama sanifu zilizokokotolewa na mfumo wa kompyuta ni sawa na alama zilizokokotolewa na Kikokotozi. Hivyo hakuna dosari yoyote iliyobainika katika masomo mengine.
 Matokeo ya somo la Islamic Knowledge yaliyotangazwa awali yamerekebishwa kwa kutumia Paper mbili kama inavyotakiwa ili kuendana na mabadiliko ya Fomati ya somo hilo. Marekebisho hayo yaliridhiwa na Baraza la Mitihani katika Kikao chake Maalum kilichofanyika tarehe 31/05/2012. Aidha, Kikao kati ya wajumbe wa Baraza la Mitihani na wawakilishi wa Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu kilifanyika tarehe 31/05/2012 ambapo walielezwa kuwa Wakuu wote wa Shule wenye watahiniwa waliofanya somo la Islamic Knowledge wataandikiwa barua rasmi kufahamishwa kuhusu marekebisho yaliyofanyika na barua hizo ziliandikwa tarehe 01/06/2012. Pia walifahamishwa kuwa matokeo yao yote ya masomo mengine hayana dosari yoyote na yanabaki kama yalivyotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania. Matokeo hayo yamewekwa kwenye tovuti ya Baraza la Mitihani na pia yatatangazwa kwenye magazeti.
 Pamoja na marekebisho hayo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itaunda Kamati ya wataalamu kuiwezesha serikali kujiridhisha zaidi na hatua zilizochukuliwa na Baraza la Mitihani ili kuepuka dosari ya aina hiyo isijitokeza tena kwa siku zijazo.
 Viongozi wa Baraza la Wakuu wa Shule za Kiislamu waliridhika na hatua zilizochukuliwa na Wizara na wameandika barua ya kuishukuru Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu namna walivyoshughulikia malalamiko yao.
4.0 HATMA YA WANAFUNZI WALIOREKEBISHIWA MATOKEO KATIKA MAOMBI YA KUJIUNGA NA VYUO VIKUU
Wizara inapenda kuwahakikishia watahiniwa waliorekebishiwa matokeo yao kwamba, kwa kuwa zoezi la usajili bado linaendelea hadi tarehe 30/06/2012, waliorekebishiwa matokeo yao watapata fursa ya kuwasilisha maombi ya kujiunga na vyuo vikuu endapo wana sifa stahiki. Aidha, kwa upande wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, maombi ya mikopo hufanyiwa kazi rasmi baada ya Tume ya Vyuo Vikuu kukamilisha mchakato wa udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu. Hivyo, hapatakuwa na athari yoyote kwa watahiniwa husika kupata mikopo endapo watakidhi vigezo vinavyotakiwa.

5.0 HITIMISHO
 Napenda kuhitimisha kwa kuwasihi wazazi, walezi, wanafunzi na jamii kwa ujumla kuwa na imani na Baraza la Mitihani la Tanzania kama chombo chetu chenye dhamana kisheria ya kuendesha mitihani nchini. Hapakuwa na hujuma yoyote iliyofanyika kwa watahiniwa ambao matokeo yao yamerekebishwa. Kosa lililojitokeza ni la kibinadamu, halikufanywa kwa makusudi wala kwa lengo lolote la kuhujumu kundi fulani la watahiniwa. Marekebisho yameshafanyika na matokeo stahiki yameshatolewa. Aidha, uhakiki uliofanyika kwa masomo yao mengine unaonesha kuwa hakuna dosari yoyote iliyobainika katika masomo yote.
 Kutokana na dhana ya baadhi ya watu kuwa kunakuwa na upendeleo kwa baadhi ya watahiniwa wa makundi fulani katika usahihishaji napenda kuwakumbusha kuwa wakati wa mitihani, watahiniwa huandika namba zao za mitihani na siyo majina. Katika taratibu za usajili wa Baraza la Mitihani hakuna kipengele chochote kinachomtaka mtahiniwa kuonesha kabila yake, dini au itikadi ya kisiasa. Vilevile, utaratibu unaotumika kuwapata wasahihishaji huzingatia uwezo wao kitaaluma na uzoefu kazini. Aidha, katika fomu ya mapendekezo ya uteuzi wa wasahihishaji hakuna mahali popote ambapo Mkuu wa Shule hutakiwa kuonesha kabila yake, dini au itikadi ya kisiasa ya mwalimu anayependekezwa kusahihisha mitihani.

 Utaratibu unaotumika kusahihisha mitihani hautoi mwanya wa upendeleo. Katika kudhibiti uwezekano wa kupendelea mtu yeyote kila msahihishaji husahihisha swali moja tu na kisha humpatia msahihishaji mwingine asahihishe swali linalofuata. Aidha, kila msahihishaji hutakiwa kuweka vifupisho vya majina yake (initials) ili ufuatiliaji uweze kufanyika kadri itakavyohitajika. Pia uhakiki wa usahihishaji hufanyika kwa lengo la kujiridhisha na usahihi wa kazi na kuhakikisha kuwa kila mtahiniwa amepata alama anazostahili. Dosari zinazobainika zimekuwa zikirekebishwa katika mchakato wa usahihishaji na wasahihishaji wanaobainika kuhusika na dosari hizo wamekuwa wakichukuliwa hatua stahiki mara zinapobainika.
 Pamoja na hayo niliyoyaeleza nina taarifa kuwa yanapangwa maandamano ambayo yanalenga suala hili hili la kutoridhika na matokeo ya awali ya somo la Islamic knowledge. Kwa kuwa suala hili limeshapatiwa ufumbuzi, nawasihi wananchi wajiepushe kushiriki maandamano hayo kwa sababu suala la msingi lililo wafanya watake kuandamana limeshatolewa maelezo. Hivyo, maandamano hayo hayatakuwa na tija.

IMETOLEWA NA DKT SHUKURU JUMANNE KAWAMBWA
WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TAREHE 07/06/2012

No comments:

Post a Comment