Wednesday, October 24, 2012

LOAN BOARD; SERIKALI YA TANGAZA KUIVUNJA BODI YA MIKOPO


HAYA SASA, KALE KAMJENGO NDIO IMEFIKIA HIVI

Serikali kuivunja Bodi ya Mikopo
NA RICHARD MAKORE
24th October 2012

Serikali imesema inafikiria kuifumua na kuivunja Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa kuwa imeshindwa kukidhi matarajio ya serikali pamoja na Watanzania wengi kama ilivyotarajiwa wakati inaanzishwa.

Bodi hiyo licha ya kupewa zaidi ya Sh. trilioni moja tangu ilipoanzishwa mwaka 2005 hadi sasa, lakini imeshindwa kuweka mkazo ili kuhakikisha inawabana watu wote waliopata mikopo walipe madeni yao ili fedha hizo zitumike kuwakopesha wanafunzi wengine wanaozihitaji.

Aidha, kwa kipindi kirefu utendaji wa bodi hiyo umekuwa hauendi sawa sawa na kumekuwa na malalamiko mengi katika utoaji wa mikopo katika vyuo vikuu.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestine Gesimba, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

“Kwa sasa idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo hapa nchini kwa ajili ya elimu ya juu ni 300,000, lakini hali ipo hivi sasa huko tuendako idadi hiyo ikifikia 500,000 na kuendelea itakuwaje?” Alihoji Gesimba.

Aliambia kamati hiyo kuwa mpaka sasa HESLB imekusanya Sh. bilioni 20 kati ya Sh. bilioni 39 ambazo zinatakiwa kukusanywa na kwamba hayo ni mapungufu makubwa ya kiutendaji.

Gesimba alisema kwa sasa kuna vyuo 50 vya elimu ya juu ambavyo vinahudumiwa na HESLB na kwamba kila mwaka mahitaji yanazidi kuongezeka.

Hata hivyo, Gesimba alisema bajeti ya elimu ya juu inazidi kupungua ingawa idadi ya wahitaji inaongezeka kila mwaka na kwamba hiyo ni moja ya changamoto zinazoikali wizara yake.

Alisema serikali imempa kazi mshauri mwelekezi kwa ajili ya kufanya utafiti kuhusu matatizo katika utoaji wa mikopo na changamoto zake ili aweze kuishauri wizara.

Aliongeza kuwa mtalaamu aliyepewa kazi hiyo tayari amemkabidhi rasimu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, na kwamba mpango mzima ukikamilika serikali itapata njia sahihi ya utoaji wa elimu ya juu nchini.

“Huyu mtalaamu atatuambia namna ya kupata vyanzo vya mapato vitakavyosaidia wanafunzi kusoma, namna ya kukusanya mikopo kutoka kwa wanafunzi walimaliza vyuo ambapo walipa mikopo pamoja na utendaji mzima, lakini hayo yakifanyika bodi hii haiwezi kuendelea kuwepo tena,” alisema.

Akizungumzia sekta ya elimu kwa ujumla, Gesima alisema serikali inatarajia kuongeza ada kwa wanafunzi wanaosoma ualimu ngazi ya cheti kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 200,000 kwa mwaka pamoja na kuanza kutoza ada kwa ajili ya usajili wa shule binafsi za msingi na sekondari.

Alisema kwa sasa hakuna gharama yoyote inayotozwa mtu ama taasisi binafsi inapotaka kusajili shule ya msingi pamoja na sekondari na kuongeza kuwa ada ya ukaguzi kwa shule hizo nayo inatarajia kupanda kutoka Sh. 500 kwa mwanafunzi mmoja hadi Sh. 1,000 kwa mwanafunzi.

Kuhusu ubora wa ufaulu, Gesima aliesema hakuna uhusiano wa moja kwa moja na shule husika kufanyiwa ukaguzi mara kwa mara na kwamba takwimu zianonyesha shule zilizoshika nafasi 10 za mwisho ndizo zilizokaguliwa mara nyingi na kwamba zilizoshika nafasi 10 za kwanza zilikaguliwa mara chache.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo, alisema wizara hiyo imepata hati chafu ya hesabu zake na kwamba kuna haja ya serikali kujipanga ili kurekebisha dosari hizo wakati mwingine.

Alisema ni jambo la kusikitisha mpaka sasa wizara haina mfumo wa kompyuta kutambua idadi ya walimu wake na madai mbalimbali wanayoidai (Database) na kwama hatua hiyo inachangia matatizo mbalimbali katika sekta ya elimu kuendelea kuwepo.

Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo, Gesimba alikiri kwamba Database ni muhimu na kwamba wizara itaanzisha utaratibu huo.

POAC YAIJUA JUU MUHIMBILI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) imeijia juu Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa kushindwa kutunza mali zake pamoja na utunzaji mbovu wa taarifa za wagonjwa hususani mafaili na majibu ya vipimo.

Kufuatia utendaji huo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe, imeagiza hospitali hiyo kufunga ofisi za Benki ya NMB zilizopo eneo la Muhimbili kwenye kiwanja cha hospitali kwa kuwa kodi ya pango haiingii Muhimbili.

Wabunge wa kamati hiyo walifikia uamuzi huo kwa kueleza kwamba mwaka 2007/2008, POAC iliiagiza Muhimbili kurejesha eneo hilo mikononi mwake badala ya kuendelea kushikiliwa na mbia ambaye ni Regent Store.

Inadaiwa kwamba mwaka 1987 Muhimbili na Regent Store, waliingia mkataba wa ukodishaji wa eneo hilo ambao ulipaswa kumalizika baada ya miaka mitano tangu kusainiwa yaani mwaka 1992.

Badala yake, Regent Store ilidai kwamba mkataba wao wa miaka mitano ulitakiwa kuhesabiwa kuanzia mwaka 1992 ambao hata hivyo, ungeisha mwaka 1997 lakini haujasitishwa hadi sasa.

Kutokana na mkanganyiko huo, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alieleza kushangazwa na ukimya wa Muhimbili hata baada ya kutoa muda mrefu kwa mkodishaji kinyume cha mkataba.

Alisema baada ya mwaka 1997, Muhimbili walipaswa kumnyang’anya eneo, lakini cha kushangaza walikaa kimya hadi mwaka 2005 ambapo Regent Store ilikimbilia mahakamani kutaka ufafanuzi wa mkataba.

Hata hivyo, Mwanasheria wa Muhimbili, Veronica Hellar, alisema kesi iliyopo mahakamani haihusiani na uhalali wa umiliki bali ufafanuzi wa mkataba na kwamba inaendelea vizuri.

Alisema kesi hiyo namba 53/2005 imepangwa kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Desemba 3, mwaka huu na hukumu itatolewa.

Hata hivyo, Lugola alisema kesi hiyo haihusiani na agizo la kamati ambalo linaitaka Muhimbili kufunga ofisi za NMB kwa kuwa benki hiyo imekodishiwa pango kinyemela na inahesabika kama mvamizi.

Kwa upande wake, Zitto alisema kukodishwa kwa jengo hilo huku Muhimbili ikikosa kodi ni kuikosesha hospitali dola za Marekani 7,200 kwa mwezi kiasi ambacho kilithibitishwa pia na Mkurugenzi wa Fedha wa Muhimbili, Agnes Kuhenga.

Baada ya maelezo ya wabunge, Zitto aliitaka Muhimbili kufunga ofisi za NMB leo na kama haitafanya hivyo kamati yake itaenda kufunga ofisi hizo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Muhimbili, Profesa Joseph Kuzilwa, aliiomba kamati kuahirisha agizo lake hadi Desemba 5, hukumu itakapotolewa, lakini POAC ilikataa.

Profesa Kuzilwa na Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili, Dk. Marina Njelekela, walikubali kupokea agizo hilo na kuahidi kulifanyiakazi.

Awali, POAC ilibaini kuwepo kwa utunzaji mbovu wa kumbukumbu za taarifa za wagonjwa hususani mafaili na kuchelewa kupatikana kwa majibu ya vipimo.

Lugola alisema inashangaza kwamba kuna wagonjwa wanasubiri faili lao kwa miezi sita na hata majibu inakuwa hivyo hivyo.

Alisema jambo hilo ni hatari kwa kuwa wapo wanaopoteza maisha kwa sababu tu faili halionekani au majibu yanachelewa huku akionya kuwa inawezekana kuna mgomo baridi usiokwisha kwenye hospitali hiyo.

Akijibu, Dk. Njelekela alithibitisha kuwepo kwa tatizo la upotevu wa mafaili ya wagonjwa na kwamba wameanza kulifanyiakazi kwa kuingiza taarifa za wagonjwa kwenye mfumo wa kompyuta ambao unahitaji Sh. milioni 790.

Hata hivyo, alisema hospitali inakabiliwa na tatizo kubwa la fedha na hivyo kwa sasa wanatafuta ufadhili wa wadau mbalimbali ili kutekeleza azma hiyo.

Kutokana na maelezo hayo, Zitto alisema: “Mafanya nini Muhimbili maana hata kazi ya kutunza kumbukumbu za wagonjwa hamuwezi, hivi hili nalo mnasubiri wafadhili wafanye? Kwa nini zisitoke kwenye fedha zenu za ndani?”

Akijibu, Dk. Njelekela alisema suala hilo litafanyiwa kazi na kwamba linahitaji kila daktari awe na kompyuta yake na pia katika kila wodi.

Zitto aliagiza fedha hizo zipatikane mara moja na kwamba Muhimbili iandike maombi ya fedha kwa Hazina na kutaka nakala ya barua hiyo ipelekwe kwa POAC kwa ufuatiliaji.

Katika hatua nyingine, POAC imekosoa mfumo wa uagizaji wa dawa unaofanywa na Muhimbili kwenda Bohari ya Dawa (MSD) na kueleza kwamba una mwanya mkubwa wa wizi wa dawa za serikali.

Kamati hiyo imeeleza kwamba ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2010/11 ilibaini kwamba Muhimbili imekuwa ikiagiza dawa lakini baadhi yake zinapofika hospitalini hapo hazilingani na zile zilizoagizwa.

Wajumbe wa POAC walieleza kuwa dawa au vifaa tiba ambazo hukataliwa na Muhimbili vinakuwa vimelipiwa lakini hurudishwa MSD na kwamba katika utaratibu huo kunatokea mwanya wa wizi.

Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imeahidi kukutana na MSD pamoja na Muhimbili ili kuona namna ya kutatua tatizo hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment